SAFARI YA TAIFA LA KENYA KUELEKEA MAZINGIRA ENDELEVU

Jun 09, 202512 mins read


SAFARI YA TAIFA LA KENYA KUELEKEA MAZINGIRA ENDELEVU
Tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya Kitaifa ya urejeshaji wa upandaji miti, Kenya imeandika historia kwa kupanda jumla ya miti milioni 783. Hatua hii ya kihistoria imewezekana kwa juhudi za pamoja kati ya wananchi wa kawaida, sekta binafsi, mashirika ya serikali, kampuni na taasisi mbalimbali.


Kwa mujibu wa Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu Bi. Deborah Barasa,sekta binafsi imekuwa mshirika mkubwa katika mafanikio haya. Waziri aidha amedokeza kuwa kama nchi tumeshuhudia kampuni na mashirika mengi yakiwaunga mkono wakulima wadogo kwa kuwapa miche na mafunzo ya upandaji miti. Hii imechochea ushiriki wa wananchi kwa wingi na kuifanya kampeni hii kuwa ya kipekee.

Katika makala haya, tunachunguza kwa undani umuhimu wa upandaji miti, mbinu bora zinazotumika na faida ambazo taifa linapata kutokana na juhudi hizi.


Miti: Msingi wa Maisha na Mazingira Bora
Miti ni hazina isiyokuwa na kifani kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine. Kwa mujibu wa
wataalamu wa mazingira, miti ina faida zaidi ya mia moja. Hifadhi ya mazingira, uboreshaji wa ardhi, makazi ya viumbe, uhifadhi wa maji na rasilimali, hewa safi na faida za kiuchumi ni baadhi ya manufaa ya moja kwa moja.


Miti hufyonza dioksidi kaboni kutoka angani na kutoa oksijeni tunayovuta kila siku. Katika zama hizi za athari za mabadiliko ya tabianchi, upandaji miti una nafasi ya kipekee katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu na kulinda sayari yetu.
Lakini si hayo tu – mizizi ya miti huzuia mmomonyoko wa udongo, huongeza rutuba na kuhakikisha mashamba yanabaki kuwa na tija. Kwa mfano, ardhi ya mkulima inayozungukwa na miti huwa na unyevu na rutuba zaidi, ikilinganishwa na maeneo yaliyonyauka.


Makazi ya Viumbe Hai
Katika misitu na maeneo yenye miti mingi, maisha ya wanyama na ndege yanastawi. Ndege kama bundi,mwewe, njiwa na hata nyani, hupata hifadhi na chakula kutokana na miti. Hii inaonesha wazi kuwa upandaji miti huimarisha bioanuwai na mfumo mzima wa maisha.


Maji, Dawa na Kipato
Miti huchangia katika kuhifadhi maji ardhini, kuvuta mvua na kuwezesha kilimo. Kwa wakulima, hili
linamaanisha msimu thabiti wa kilimo na mavuno ya kutegemewa. Aidha, jamii nyingi hupata kipato kutokana na bidhaa za miti – matunda, dawa za asili kutoka mizizi, majani na magamba, pamoja na mbao na kuni.

Watafiti wa afya ya jamii wamebaini kuwa watu wanaoishi karibu na mazingira ya kijani na miti wana uwezekano mkubwa wa kuwa na afya bora. Hewa safi huongeza ubora wa maisha na hupunguza magonjwa yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira.


Mbinu Bora za Kupanda Miti
Faida hizi zote haziwezi kupatikana bila kufuata mbinu sahihi za upandaji. Mbegu lazima zichaguliwe kulingana na hali ya hewa, mwangaza na upatikanaji wa maji katika eneo husika. Ardhi inapaswa kuandaliwa kwa kuondoa magugu, kupalilia na kuhakikisha udongo una rutuba.


Shimo la kupanda linapaswa kuwa na kina kinachofaa, na nafasi ya kutosha kati ya miti kuhakikisha kila mti unakua vizuri. Baada ya kupanda, mti unahitaji maji ya kutosha, ulinzi dhidi ya wadudu na kuendelea kuangaliwa hadi ukomae.


Upandaji wa miti si jukumu la serikali pekee – ni wajibu wa kila Mkenya. Kila mti unaopandwa ni hatua moja mbele kuelekea Kenya iliyo na mazingira bora, afya njema, na uchumi unaozingatia maadili ya maendeleo endelevu.
Katika kila kijiji, mtaa na taasisi, kampeni hii inaweza kuleta mabadiliko ya kweli. Kwa pamoja, twendelee kupanda miti-kwa kizazi kijacho, na kwa mustakabali wa taifa.

Imeandikwa na,

Bint Kombo.